Qur'an Tukufu: "Mwenyezi Mungu huzichukua nafsi wakati wa kufa kwake, na ambazo hazijafa katika usingizi wake…"
Shirika la Habari la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Dar-es-Salaam, Inna Lillah wa Inna Ilayhi Rajiun - Wanafunzi na Walimu wa Jamiat Al-Mustafa (s) - Mbezi Beach, Dar es Salaam, leo hii baada ya Sala ya Dhuhrain, wamepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Sheikh wa Umma wa Watanzania, Mpenzi na Mfuasi wa Mtume Muhammad (s.a.w.w) na Aali zake (a.s), Sheikh Yasin Idi Bashemera (Mwenyezi Mungu Amrehemu).
Kwa pamoja wamekusanyika na kusoma Surat Yasin wakimuombea marehemu dua ya maghfira na rehma za Mwenyezi Mungu, ili ampokee kwa utukufu wake na amuweke pamoja na kizazi kitukufu cha Mtume Muhammad (s.a.w.w), yaani Ahlul-Bayt (a.s).
Wanafunzi na Walimu kwa pamoja walinyanyua mikono yao kwa unyenyekevu, wakiomba kwa baraka za kisomo cha Surat Yasin, na kwa Heshima na Utukufu wa Mtume Muhammad (s.a.w.w) na Ahlul-Bayt wake Watoharifu (a.s), Mwenyezi Mungu amsamehe madhambi yake, na amzidishie katika mema yake, na alifanye kaburi lake kuwa na nuru angavu isiyo na mwisho.
Kwa hisia za machozi na mshikamano wa undugu wa imani, pia waliwaombea watoto wa Marhumu Sheikh Yasin uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu cha kumkosa baba yao kipenzi, wakimuombea pia marehemu baraka na kheri katika maisha yake ya Barzakh.
Mwenyezi Mungu anasema katika Qur’an Tukufu:
"اللَّهُ يَتَوَفَّى الْأَنفُسَ حِينَ مَوْتِهَا وَالَّتِي لَمْ تَمُتْ فِي مَنَامِهَا ۖ فَيُمْسِكُ الَّتِي قَضَىٰ عَلَيْهَا الْمَوْتَ وَيُرْسِلُ الْأُخْرَىٰ إِلَىٰ أَجَلٍ مُّسَمًّى ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يَتَفَكَّرُونَ".
(Mwenyezi Mungu huzichukua nafsi wakati wa kufa kwake, na ambazo hazijafa katika usingizi wake… - Az-Zumar: 42).
Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Muweza juu ya kila kitu.
Walhamdulillahi Rabbil-‘Aalamin.
Your Comment